Mtaji mkubwa wa Biashara ya Mtandao sio pesa, mtaji mkubwa ni jinsi ya kujua kutumia muda wako vizuri, jitihada pamoja na mtaji watu ambao wanakuzunguka ujue jinsi ya kuwashirikisha.
Hapa nakushirikisha baadhi ya hatua mhimu nilizotumia mimi kuchagua ni kampuni gani inanifaa kufanya nayo biashara ili niweze kufikia malengo yangu, na hivi ndio vigezo mhimu vya kuzingatia.
Jinsi ya kuanza biashara ya Mtandao(Network marketing)
*HATUA YA KWANZA.
Kwanza ifahamu maana ya Biashara ya mtandao.
Kuna tofauti ya neno mtandao linalotumika hapa katika biashara hii mpya na neno “mtandao” kama linavyotumika katika upande wa mawasiliano.
Katika Biashara ya Mtandao (Network Marketing), neno mtandao linamanisha “jumuia, timu au kikundi cha watu ambacho kimeungana na kinaendelea kupanuka kwa idadi ya watu kuongezeka kwa lengo la kila mtu aliopo katika timu na anayejiunga kumiliki biashara yake kama wakala wa kujitegemea katika kampuni husika.
Kufahamu zaidi maana halisi ya biashara ya Mtandao soma sehemu ya kwanza ya hii makala (hapa )
* Chagua kampuni ya Biashara ya Mtandao(Network Marketing) inayokufaa.
Kujua kama kampuni inakufaa au la, ipime kupitia vigezo vifuatavyo:
a) Uimara na Muda wa kampuni tangu kuanza.
Angalia uimara wa kampuni kiuchumi, jinsi inavyokuwa kiuchumi tangu ianze na pia muda (umri) wake tangu ianze kufanya biashara ya mtandao. Ikiwa kampuni si imara kiuchumi na ni changa unaweza kujiunga na kuanza biashara lakini kufanya hivyo unakuwa unaongeza hatari ya kupoteza muda na pesa yako kama kampuni itaporomoka zaidi na kushindwa kutoa malipo, kujiunga katika kampuni lililo dumu angalau miaka mitano ni vizuri zaidi kwa sababu linakuwa limesimama kiuchumi.
Kuna wengine hupenda kujiunga makampuni mapya kwa sababu yanakuwa hayajajulikana sana hivyo ni rahisi watu kuingia. Mimi kuna makampuni mengi nilipata kuyahudhuria semina zake lakini sikujiunga kwa sababu mengine niliona mimi ndio naenda kuinua kampuni badala ya kampuni kuniinua.
b) Bidhaa zinazotumika na kampuni kuendesha biashara.
Angalia, bidhaa za kampuni unayotaka kufanya nayo biashara kama ni:
Bidhaa ambazo ni Tangible (ziwe za kushikika);
Nilipoamua kuanza hii biashara nilichagua kampuni ambayo ina bidhaa za kuonekana machoni mwa watu. Nilitambua jamii inayonizunguka ni vigumu kuamini biashara yangu kama nitakuwa natoa stori kuwa nina kampuni linafanya biashara. Wachache wangeniamini. Mara nyingi makampuni ambayo ya najihusisha na biashara bila ya kuwa na bidhaa yanakuwa katika mfumo wa pyramid scheme mfano wa DECI, ndio maana unashauriwa kuwa na kampuni lenye bidhaa za kushikika.
Bidhaa za kutumika na kuisha
Ikiwa kampuni ina bidhaa ambazo mteja akinunua leo anatumia miaka mitano au hadi iharibike ndio akutafte tena; bidhaa za namna hii utabaki kutafta kila siku wateja wapya. Lakini bidhaa za kutumika na kuisha, kama Sabuni, Dawa, Mbolea, Mafuta n.k hivi mteja atavihitaji kila wakati, kwanza ni mhimu katika maisha ya binadamu na pili vinatumika na kuisha hivyo mteja anarudi tena na kama bidhaa ni nzuri atakuletea na wateja wengine. Jiulize unafanya biashara ya kutengeneza timu biashara ambayo hata mtu aliopo kwenye timu yako akinunua kitu kwa matumizi yako utalipwa; je kama ni bidhaa za kukaa hadi mwaka ikinunua atarudi kununua lini?
Bidhaa zenye ubora na za kipekee.
Si rahisi kufanya biashara na bidhaa ambazo zimetapakaa kila mahali, lazima bidhaa za kampuni yako ziwe ni unique hata kama zipo zinazofanana na hizo bidhaa lakini ziwe na utofauti flani katika ubora na vitu vingine ambavyo vitafanya mteja aache bidhaa ya kawaida anunue yako.
Bei ya bidhaa unazotumia kufanyia biashara.
Je, bei ya bidhaa anayotakiwa kulipa mteja anaweza kuimudu au inaendena na ubora wa bidhaa? Sio lazima bidhaa iwe bei ya chini au juu ndio inunuliwe. Bei ya bidhaa iendane na ubora wa bidhaa na mahitaji ya watu ili bidhaa ziweze kuuzika. Hiki ni moja ya vigezo vilivyonisaidia kufurahia hii biashara, kigezo hiki kilinisaidia kwa mara ya kwanza niliochukua bidhaa chache za kuanzia, nilichukua kama aina 3, lakini kuna bidhaa ambazo ziliisha ndani ya siku 3 hadi nilijilaumu kwa nini sikuchukua nyingi, sabuni na pedi ziliisha ndani ya siku mbili, bei ya sabuni niliuza kwa shilingi 3,500 hadi 5,000.
Pia ni vyema kampuni unayofanyia biashara kwa asilimia kubwa iwe inazalisha bidhaa zake yenyewe badala ya kutegemea toka makampuni mengine.
Angalia Mfumo wa malipo na uundaji wa timu jinsi ulivyo wekwa(compesation plan/marketung plan)
Mifumo ya malipo ipo tofauti kwa kila kampuni na utaratibu jinsi unavyoweza kuunda timu na watu wako watakavyo unda timu na namna watakavyo panda ngazi.
Pia utaratibu na mfumo wa kupokea malipo kutokana na manunuzi yako binafsi na timu yako.
Mifumo hii huandaliwa na kampuni husika, mfanyabiashara unakuwa huna mamlaka ya kuibadili lakini inatakiwa ijulikane kabisa ili kila wakala au mfanyabiashara kupitia kampuni husika ajue akifanya hiki analipwa kiasi kadhaa, akiwa daraja flani atalipwa shilingi kadhaa kutokana na daraja lake na timu yake na manunuzi yake.
Ndugu,nikwambie kwa sababu sikuwa na pesa nyingi ya kuwekeza katika biashara hii kwa kuwa makini katika kigezo hiki niliweza kupanda level na kuongeza malipo toka asilimia 5 hadi 25 ya malipo nayopata toka kwa kampuni huku nikiwa nimetumia jumla ya fedha isiyozidi laki 4 tangu nilipojiunga ukijumlisha na pesa ya kujiungia elf 26 niliotoa, nilikuwa makini katika kuamua ni kampuni gani niwekeze pesa yangu kidogo niliokuwa nayo na muda wangu; na ndivyo mjasiriamali mali unatakiwa kuwa makini.
Kianzio (stater kit) wakati wa kujiunga na kampuni yako ya biashara.
Ikiwa gharama ya kujiunga ipo juu sana lakini wewe una uwezo wa kujiunga utajiunga na kuanza biashara lakini, watu wengine watashindwa kujiunga na wewe kufanya biashara badala yake watatafuta kampuni nyingine wanayoimudu watajiunga huko japo wanapenda kujiunga katika kampuni yako au timu yako.
Angalia kama kuna gharama za kufunga mwezi.
Kuna wakati niliajiriwa serikalini, mshahara ukachelewa takribani miezi mitatu, hapa ndio niliona umhimu wa kuwa na kampuni ambalo lina vigezo nafuu vya manunuzi, pesa niliokuwa nayo ndio ilikuwa inatumika kula na kuendeshea biashara, kuna mwezi nilifanya manunuzi ya shilingi elfu 7 tu lakini mwisho wa mwezi nililipwa pesa yangu ya manunuzi pamoja na watu walio katika timu yangu.
Makampuni mengi yana kiwango cha kufanya manunuzi kulingana na daraja uliopo ili ukidhi vigezo vya kulipwa kwa mwezi au wiki husika.
Jaribu kuangalia kama kampuni limeweka vigezo kama hivyo, je ni rafiki kwa mfanya biashara ili usije unajikuta kila wiki au mwezi unalazimika kufanya manunuzi hata kama huna cha kulipwa au mteja unaambulia faida ya kuuza tu.
Ni vema pia ukahakikisha kuna mfumo mzuri wa kupata elimu juu ya biashara.
Angalia kama kampuni lina ushirikiano kati ya waliotangulia na waliochini(wafanyabiashara wachanga); lazima kampuni iwe na mfumo mzuri wa waliotangulia (upline) kutoa elimu kwa wafanyabiashara wachanga(downline)
Kuna mtu mmoja aliwahi kuhama toka kampuni aliokuwepo,nikamweka kwenye grup la Whatsapp alifrahia akasema yaani sasa ndio naona utamu wa biashara ya mtandao hapa nauliza swali najibiwa na watu, njia nafundishwa kilichobaki ni juhudi tu.
Pia kuwepo vitu kama; CD na Majarida elekezi jinsi ya wa wewe wakala wa kampuni unavyoweza kuendesha biashara na pia ufafanuzi wa bidhaa kama kampuni lina bidhaa.
CD, Video na Majarida yenye sura ya kampuni na ukifungua ndani kumejaa historia ya kampuni na picha za viwanda kuonesha jinsi namna bidhaa zinavyotengenezwa tu bila maelezo ya jinsi unavyoweza kuendesha biashara yako ujue hayata kusaidia sana. Na kama imetokea umejiunga na kampuni la namna hii huna budi kuambatana bega kwa bega na upline wako aweze kukupa mwanga wa kutosha kuweza kunyenyuka. Kwa bahati mbaya kampuni niliojiunga nayo vitabu vyake na CD zilikuwa katika mfumo huu. Lakini kulikuwa na ushirikiano wa kuhakikisha kila member mpya anapata maarifa hadi kusimama.
*HATUA YA PILI
Kujiunga na kampuni na kuanza biashara yako.
Baada ya kuwa umepata kampuni ukaamua kutoa pesa ya kuanzia (starter kit) kwa wakala atakae kudhamini kupitia timu yake au ukalipia moja kwa moja ofisi ya kampuni ilio karibu nawe; baada ya uthibitisho katika kampuni ukapata Kitambulisho na au Namba ya uwakala tayari wewe ni wakala na mfanyabiashara, sio kwamba kampuni imekuajiri bali wewe ndio umejiajiri kumiliki biashara kupitia kampuni husika. Unatakiwa kuanza kuendesha biashara yako na kuhakikisha inakuletea mafanikio makubwa ndani ya muda ulojiwekea.
“Nini ufanye baada ya kuwa umeanza biashara ya mtandao ili uweze kupata faida na kusimama haraka”
* Wekeza katika biashara yako, wekeza muda, jitihada na jinsi yakuwashirikisha watu fursa ulionayo.
Unapokuwa tayari ndani ya safari ya mafanikio katika biashara yoyote lazima uihangaikie iweze kukua nakukupa matunda mazuri.
Biashara ya Mtandao ina sifa za kipekee ambazo ni rahisi mtu yeyote mwenye sifa za ujasiriamali anaweza kuifanya tofauti na biashara zingine.
Hakikisha unatenga muda baada ya kazi zako au masomo kwa wiki au kila siku kadri unavyoweza kupata muda wa ziada, muda huu unaweza kuhamisha toka muda wako ambao unatumia kupiga stori na marafiki zako au kuchati katika mitandao ya kijamii badala ya kuchati stori ambazo hazikuingizii pesa hamia sasa na kujiunga na magrup ya biashara yaliopo Whatsapp, Facebook, Twitter, Instagram, n.k utangaze biashara yako. Badala ya mitandao hii kuendelea kukuchukulia pesa kwa kununua vifurushi vya internet (mtandao) unaweza itumia sasa kuingiza pesa.
Hizo ni moja ya njia mhimu nilizotumia nikapiga hatua na ndizo watu waliofanikiwa hadi kuingiza zaidi ya milioni kwa mwezi katika hii biashara huzingatia. Hii ni biashara ya kufanya ukiwa nyumbani hivyo lazima uache kujitwisha zigo la kuendesha biashara km wafanyavyo machinga na wafanyabiashara wa kawaida.
Muda ulionao sasa ukiitumia vizuri utakupa manufaa makubwa mbeleni, muda ndio huu usiache kufungua miradi ukijiahidi nikimaliza chuo au ukistaafu kazi utafanya km inawezekana sasa fanya, wekeza katika biashara ambazo hazihitaji usimamizi wa moja kwa moja kama huna muda wa kusimamia.
Ukiwa unaendelea kutumia muda wako unaobaki Kufanya biashara ukiwa nyumbani baada ya kazi au shughuli zako pia kumbuka kujifunza, biashara ni maarifa.
Jifunze jinsi ya kuendesha biashara yako na kujenga timu toka kwa watu waliokuunganisha na biashara katika kampuni yako pia jenga utamaduni wa kujisomea vitabu vya biashara na kuongeza kipato, video na vitabu. Hivi vipo vya bure na vya kulipia katka hard copy na soft copy unaweza kudownload kutoka katika mtandao au ukanunua.
Vitabu vyangu vya kwanza kusoma nikiwa katika biashara hii ni:
Four Quadrants (The Guidance To Financial Freedom)
Business Of 21st Century pamoja na
How to build Multi Level money machine.
Japo nilikuwa na nipo katika ajira nafanya kazi kuanzia saa 1 na nusu asubuhi hadi saa kumi jioni, bado nilijitahidi, nilijali biashara yangu na kutenga muda wa kujifunza , kama na wewe ukiijali biashara yako na ukawa unaitangaza na kushirikisha watu unakuwa unastawisha biashara yako na kuifanya ianze kuchanua na kustawi kama mti mchanga unaostawi unapopata lishe na mwanga matunda utayaona baada ya muda.
(BAADA YA MUDA NITANZA KUWEKA VITABU KATIKA MFUMO WA PDF KWENYE WEBSITE HII, UTAFUNGUA PAGE YA PRODUCTS NA KU_DOWNLOAD)
Ushauri mwigine, ni vema ukajenga utaratibu wa kuwa unawekeza pesa kulingana na kipato chako na malengo yako, jitihada kufanya manunuzi hata mara moja kwa mwezi hii itakusaidia kupanda daraja. Ukiuza mzigo usile pesa km umeanza na kianzio kidogo sana, acha pesa iendelee kuzunguka, hadi biashara itakapoanza kujiendesha. Hili ni muhimu kama unakuwa umeanza na mtaji kidogo sana.
Nakumbuka mimi nilianza na elfu 80, lakini nikijitahidi hadi mtaji ukafika laki 3 na elfu 80.
Anza kuwekeza katika rasmali watu, biashara zilizosambaa duniani na kukua zimejengwa juu ya rasmali watu.
Makampuni, Taasisi na Jumuia mbalimbali zote zimejengwa kwa kuunganisha watu.
Katika biashara unapokuwa na mtaji mkubwa wa watu (social capital) au soko kubwa ndivyo na faida inakuwa kubwa. Hakikisha unaanza taratibu kujenga mtandao imara wa kibiashara kwa kushirikisha watu biashara yako.
Biashara ya kufanya peke yako haina matunda makubwa ukilinganisha na makampuni au jumuia zinazoendeshwa na timu ya wafanyakazi wengi ndio maana kila kampuni linapokuwa hujitahidi kufungua milango ya ajira na wafanyakazi huongezwa na matawi yanafunguliwa sehemu mbalimbali faida inaendelea kuwa kubwa.
Sasa biashara ya mtandao inakupa nafasi ya kumiliki biashara kubwa kwa gharama ndogo, utafanya biashara na idadi ya watu unaotaka, na kama matawi utaweka kila sehemu unayotaka duniani, bila kikwazo chochote unakuwa ni sawa na mtu anaejenga kampuni au jumuia na yenye matawi sehemu mbalimbali.
Faida za kutengeneza timu (network) ukiwa katika hii biashara.
Unapokuwa na timu ni sawa na mmiliki wa kampuni yenye wafanyakazi na yenye matawi sehemu mbalimbali. Tofauti ni katika mfumo wa kawaida unalazimika kuwalipa lakini katika mfumo huu kila mtu anakuwa amejiajiri na anasimama yeye kama yeye.
Kuwa na timu kuna kutengenezea na kukuingizia kipato kizuri ambacho hakina kikomo aina ya Passive Income, mbali na kile utakachopata wakati ukiuza bidhaa.
Mfano:
Unapoanza hii biashara unakuwa upo mmoja. Unapokuwa mmoja katika hii biashara unapata faida mbili tu:
a) Faida utakayolipwa na kampuni kwa manunuzi uliofanya.
b) Faida utakayouza mzigo utakaokuwa umenunua.
Hapo unapokuwa mmoja unakuwa sawa na mjasiriamali wa chini hadi ufanye ufanye wewe manunuzi au uuze ndio upate faida.
Lakini unapokuwa na timu yenye watu sehemu mbalimbali, pale mmoja wenu anapokosa soko la bidhaa flani mwingine atauza alipo na kila anaefanya biashara katika timu yako ni sawa na wewe umefanya; kampuni itakulipa faida kulingana na mfumo wa malipo uliopo.
Timu yako inajumuisha watu unaowapata wewe na wengine wanaokuja kujiunga kufanya biashara kwa watu walio tayari kwenye timu yako.
Hivyo timu itaendelea kukua siku hadi siku hata km wewe hutakuwa unaingiza watu wapya lakini ulioleta mwanzo na walioletwa na timu yako wataendelea kuingiza watu, kadri mnavyokuwa wengi na kama baadhi yenu au wote mnafanya biashara na malipo pia huongezeka.
Kuwa na timu kuna kujengea kipato ambacho utaanza kukipata pasipo kikomo, hii ni biashara ya kulenga mbeleni baada ya muda wa mwaka mmoja na kuendelea unakuwa na timu kubwa na unaingiza faida hata ikitokea una matatizo hujauza mwezi mzima.
Angalia jinsi ya kuanza biasharana mtaji kati ya TZS26,000/= na TZS400,000/=
Mwisho, hakuna biashara ambayo utajifunza mbinu zote na ukamilike asilimia mia moja huku ukiwa bado hujaianza biashara husika, unapokuwa ndani ya biashara ndio unaendelea kujifunza mbinu mpya kutoka kwa wenzako na changamoto unazokuwa unakabiliana nazo kila siku. Biashara haina mwisho wa kujifunza.
Nakutakia Mafanikio Mema